1Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akisali. Alipomaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tunakuomba utufundishe kusali kama Yohane mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake.” 2Yesu akawaambia, “Mnaposali, semeni: Baba! Jina lako litukuzwe; Ufalme wako ufike. 3Utupe daima chakula chetu cha kila siku. 4Utusamehe dhambi zetu, maana sisi tunawasamehe wote waliotukosea; wala usitutie katika majaribu.” 5Kisha akawaambia, “Tuseme mmoja wenu anaye rafiki, akaenda kwake usiku wa manane, akamwambia: Rafiki, tafadhali niazime mikate mitatu, 6kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa. 7Naye, akiwa ndani angemjibu: Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe! 8Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji. 9Kwa hiyo, ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa. 10Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye hufunguliwa. 11Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki? 12Na kama akimwomba yai, je, atampa ng'e? 13Ninyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Basi, baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba.” 14Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea hata umati wa watu ukashangaa. 15Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anamfukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” 16Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonyesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. 17Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliofarakana wenyewe, hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yeyote inayofarakana huangamia. 18Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? 19Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu ninyi. 20Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. 21“Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. 22Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. 23Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. 24“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu fulani, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzikia. Asipopata, hujisemea: Nitarudi kwenye makao yangu nilikotoka. 25Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. 26Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba waovu zaidi kuliko yeye; wote huenda na kumwingia mtu yule. Hivyo, basi hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko pale mwanzo.” 27Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri tumbo lililokuzaa, na maziwa yaliyokunyonyesha!” 28Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.” 29Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona. 30Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. 31Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atashuhudia kwamba kina hatia. Yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni; kumbe hapa pana mkuu zaidi kuliko Solomoni. 32Watu wa Ninewi watatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, na watashuhudia kwamba kizazi hiki kina hatia. Hao watu wa Ninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na hapa pana mkuu zaidi kuliko Yona! 33“Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa pishi, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga. 34Jicho lako ni kama taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza. 35Uwe mwangalifu basi mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza. 36Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utang'aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.” 37Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. 38Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa. 39Bwana akamwambia, “Ninyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. 40Wapumbavu ninyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? 41Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu. 42“Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine. 43“Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. 44Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.” 45Mmoja wa walimu wa Sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.” 46Yesu akamjibu, “Na ninyi walimu wa Sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku ninyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia. 47Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua. 48Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao. 49Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine. 50Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu; 51tangu kumwagwa damu ya Abeli mpaka kifo cha Zakariya ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, hakika kizazi hiki kitaadhibiwa kwa matendo haya. 52“Ole wenu ninyi walimu wa Sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; ninyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie.” 53Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na walimu wa Sheria wakaanza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi 54ili wapate kumnasa kwa maneno yake.