1Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao. 2Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa. 3Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake. 4Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni. 5Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: “Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako.” 6Alisema pia mahali pengine: “Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” 7Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu. 8Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso. 9Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii, 10naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki. 11Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa. 12Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa. 13Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini. 14Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.